Wasimamizi Wakuu wa Vituo vya Kupigia Kura pamoja na Wasimamizi Wasaidizi wameanza rasmi mafunzo ya siku mbili yanayofanyika katika Shule ya Sekondari Madaba, yakilenga kuwaandaa kwa majukumu yao kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Katika siku ya kwanza ya mafunzo hayo, washiriki walikula viapo vya utunzaji siri na kujitoa katika vyama vya siasa, ikiwa ni sehemu ya matakwa ya kisheria yanayohakikisha uadilifu na usawa katika usimamizi wa uchaguzi.
Akifungua mafunzo hayo, Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi wa Jimbo la Madaba, Wakili Abdul M. Manga, aliwataka Wasimamizi na Wasaidizi wao kutekeleza wajibu wao kwa weledi, uadilifu na kutokuegemea upande wowote wa chama cha siasa.
“Ni muhimu msichukulie uchaguzi kama jambo la mazoea, bali kama dhamana kubwa mliyopewa na Taifa. Zingatieni Sheria, Katiba na miongozo yote ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ili kuhakikisha mchakato wa uchaguzi unafanyika kwa haki na amani,” alisema Wakili Manga.
Akinukuu Kifungu cha 20 cha Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya mwaka 2024, Wakili Manga alikumbusha kuwa mtu yeyote anayeajiriwa na Tume kwa kipindi cha uchaguzi atachukuliwa kuwa mtumishi wa Tume na hivyo anapaswa kuzingatia maadili, Katiba na sheria za tume.
Aliwataka Wasimamizi hao kuwahudumia wapiga kura wote bila ubaguzi, hususan makundi yenye mahitaji maalumu kama wazee, wajawazito, watu wenye ulemavu na wagonjwa, akisisitiza umuhimu wa kuwapa kipaumbele katika siku ya kupiga kura.
Katika mafunzo hayo, washiriki walipata fursa ya kujifunza mada mbalimbali ikiwemo ufungaji wa vituturi na masanduku ya kura, matumizi ya majalada ya nukta nundu, na upangaji sahihi wa vituo vya kupigia kura. Pia walitazama video za mafunzo kuhusu namna ya kukunja karatasi ya kura na taratibu za msingi za usimamizi wa kituo.
Washiriki walipata nafasi ya kuuliza maswali, kujadili changamoto na kubadilishana uzoefu, huku wakiahidi kufanya kazi kwa uadilifu, uwazi na uaminifu bila kuegemea chama chochote cha siasa.
Mafunzo hayo yanaendelea kesho kwa awamu ya pili, ambapo mada nyingine muhimu zitajadiliwa ili kuhakikisha Wasimamizi wote wako tayari kikamilifu kusimamia uchaguzi kwa umakini na ufanisi.



MADABA - RUVUMA
Anwani ya Posta: 38 BARABARA YA KIFAGURO MAGINGO, P.O.BOX 10, 57186 MADABA, SONGEA
Simu: 0252951052
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@madabadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Madaba.Haki zote zimeifadhiwa