WAHITIMU WA UFUNDI STADI KUPATIWA VIFAA VYA KUANZIA KAZI VYENYE THAMANI YA MILIONI 4.4 Hope Village Organisation Yaendeleza Huduma kwa Watoto wa Mazingira Hatarishi Ruvuma.
Katika juhudi za kuwawezesha vijana kujiajiri na kujitegemea kiuchumi, Asasi ya Ushirika wa Kijiji cha Matumaini (Hope Village Organisation) imetoa vifaa muhimu vya Ufundi Uashi na Ushonaji vyenye thamani ya jumla ya shilingi milioni 4.4. Vifaa hivyo vimetolewa wakati wa Mahafali ya pili ya chuo cha ufundi stadi ambayo imefanyika katika viunga vya taasisi hiyo mnamo Novemba 25, 2025. vifaa hivyo ni cherehani kwa kila mhitimu wa fani ya ushonaji na boksi lenye vifaa vyote muhimu kwa kazi ya ujenzi kwa kila mhitimu wa fani ya ujenzi.

Hafla hiyo ilifanyika wakati wa mahafali ya pili ya wanafunzi wa ufundi stadi, ambapo mgeni rasmi alikuwa Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Madaba, Dkt. Musa Rashid. Akizungumza kwenye mahafali hayo, Dkt. Rashid aliipongeza asasi hiyo kwa mchango wake mkubwa katika kuwawezesha vijana kupitia elimu ya ufundi na malezi yenye mwanga wa matumaini kwa jamii.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa, kila mhitimu wa Ufundi Uashi amepokea kifurushi cha zana 12 muhimu zenye thamani ya shilingi 892,500, ikijumuisha brick trowel, spirit level, wooden float, steel float, tape measure na tool box, n.k
Aidha, wahitimu wa Ushonaji watapatiwa kila mmoja cherehani moja, jumla vyerehani sita vyenye thamani ya shilingi 3,540,000, hatua itakayowasaidia kuanza safari yao ya kujitegemea kupitia ubunifu na kazi za mikono.
Katika hotuba yake, mwakilishi wa shirika alisema kuwa programu hiyo inalenga kupunguza umaskini na kukuza kipato kwa kuwapa vijana uwezo wa kujiajiri. Aliongeza kuwa mafunzo hayo yamechangia katika kutimiza malengo ya maendeleo endelevu (SDGs), hasa katika maeneo ya elimu bora, ubunifu, ajira na uchumi jumuishi.
Wakati huo huo, Hope Village Organisation inaendelea kutoa huduma za elimu na malezi kwa watoto 151 wanaoishi katika mazingira hatarishi kutoka Halmashauri ya Madaba na Manispaa ya Songea. Kati yao, 71 wanasoma shule za msingi, 35 sekondari, 19 vyuo vya ufundi stadi, 6 wa chuo vya Kati , 4 vyuo vikuu, huku 16 wakihitimu elimu ya msingi.
Wahitimu wote walikabidhiwa Living Certificates pamoja na vifaa vya msingi vya kazi kama sehemu ya kuwaandaa kuanza safari ya kujitegemea mara baada ya kuhitimu.
Hope Village Organisation ni asasi inayojishughulisha na kutoa huduma za malezi, elimu, ulinzi na mafunzo ya ujuzi kwa watoto na vijana wanaoishi katika mazingira hatarishi. Asasi hii imejikita katika kuwatunza watoto wanaoishi katika mazingira magumu, kuwapatia makazi salama, chakula, huduma za afya, msaada wa masomo, pamoja na kuwawezesha kupitia mafunzo ya ufundi stadi ili waweze kujitegemea na kujenga mustakabali bora wa maisha yao. Kupitia programu zake, Hope Village inaendelea kuwa mwanga wa matumaini kwa jamii kwa kukuza vipaji, kuimarisha stadi za maisha na kuweka msingi thabiti wa maendeleo kwa watoto na vijana wa Ruvuma na maeneo mengine.
MADABA - RUVUMA
Anwani ya Posta: 38 BARABARA YA KIFAGURO MAGINGO, P.O.BOX 10, 57186 MADABA, SONGEA
Simu: 0252951052
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@madabadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Madaba.Haki zote zimeifadhiwa