Halmashauri ya Wilaya ya Madaba leo imefanya sherehe ya kuhitimisha na kuhidhinisha Baraza la Wazee katika hafla iliyofanyika katika kijiji cha Lituta, tukio lililohudhuriwa na wazee kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya pamoja na viongozi wa serikali.
Shughuli zilianza kwa mapokezi na kuwasili kwa wazee katika eneo la tukio, yakifuatiwa na upimaji wa afya na lishe kwa wazee wote kama sehemu ya huduma za ustawi na ulinzi kwa wazee katika jamii. Upimaji huo ulilenga kuimarisha afya zao na kuwatambua wale wanaohitaji huduma za haraka.
Baada ya huduma hizo, kikao maalumu cha Baraza la Wazee kilifunguliwa rasmi, ambapo hatua ya uchaguzi wa viongozi wa Baraza ilifanyika kwa amani na uwazi. Wazee walipata nafasi ya kutoa salamu fupi, wakieleza matumaini yao juu ya ushirikiano na utendaji wa baraza jipya katika kusimamia masuala yao.
Katika hafla hiyo, viongozi wa Halmashauri walitoa makaribisho rasmi kwa wazee wote na kusisitiza dhamira ya Serikali katika kuboresha ustawi wa wazee kupitia mifumo ya uwakilishi kama Baraza la Wazee.
Tukio hilo pia liliambatana na utambulisho wa Baraza Huru la Wilaya, ambalo linalenga kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha sauti na mahitaji ya wazee yanapewa kipaumbele.
Katika kuhitimisha sherehe hiyo, Halmashauri iligawa vitu mbalimbali kwa wazee wasiojiweza ikiwa ni ishara ya kuwajali na kuwashika mkono wazee wanaokabiliwa na changamoto za kiuchumi na kijamii.
Sherehe hiyo imeacha faraja na matumaini kwa wazee wa Wilaya ya Madaba, huku viongozi wakiahidi kuendelea kuimarisha ustawi, haki na nafasi ya wazee katika maendeleo ya wilaya.
MADABA - RUVUMA
Anwani ya Posta: 38 BARABARA YA KIFAGURO MAGINGO, P.O.BOX 10, 57186 MADABA, SONGEA
Simu: 0252951052
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@madabadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Madaba.Haki zote zimeifadhiwa