Ujenzi wa nyumba nne za walimu katika Shule ya Sekondari Matetereka, Halmashauri ya Wilaya ya Madaba, mkoani Ruvuma, umekamilika kwa mafanikio makubwa. Mradi huu umegharimu kiasi cha Shilingi Milioni 201 zilizotolewa kupitia Mradi wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Akizungumza wakati wa kukagua nyumba hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba, Wakili Sajidu Idrisa Mohamed, aliwapongeza viongozi wa kijiji pamoja na walimu kwa ushirikiano mzuri waliouonesha katika utekelezaji wa mradi huo muhimu.
Wakili Sajidu aliwahimiza walimu kuanza kuzitumia nyumba hizo mara moja, akisisitiza kuwa zinatatua changamoto ya makazi kwa walimu waliokuwa wakiishi mbali na shule. Alisisitiza umuhimu wa kuzitunza nyumba hizo ili ziweze kudumu na kutoa huduma bora kwa muda mrefu.
Kwa upande wao, uongozi wa Shule ya Sekondari Matetereka umeishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kutoa fedha zilizowezesha ujenzi huo. Wameeleza kuwa nyumba hizo zitaboresha mazingira ya kazi kwa walimu na hivyo kuinua kiwango cha taaluma shuleni hapo.
Mradi huu ni sehemu ya jitihada za serikali katika kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia nchini, hasa katika maeneo ya vijijini.
MADABA - RUVUMA
Anwani ya Posta: 38 BARABARA YA KIFAGURO MAGINGO, P.O.BOX 10, 57186 MADABA, SONGEA
Simu: 0252951052
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@madabadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Madaba.Haki zote zimeifadhiwa