Halmashauri ya Wilaya ya Madaba imekabidhiwa Cheti cha Pongezi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kutokana na kutenga fedha za lishe kwa kiwango cha juu kwa mwaka wa fedha 2025/2026. Cheti hicho kimetolewa tarehe 21 novemba 2025, katika Maadhimisho ya Siku ya Lishe Kitaifa yaliyofanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Matarawe, Wilaya ya Songea.
Akizungumza katika maadhimisho hayo kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Abbas Ahmed Abbas, amesema Siku ya Lishe Kitaifa ni muhimu kwa kuwa inaikumbusha jamii wajibu wa kuzingatia ulaji bora ili kujenga taifa lenye afya imara.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Dkt. Louis Chomboko, amewasilisha taarifa ya hali ya lishe mkoani humo na kueleza kuwa kiwango cha udumavu kwa watoto chini ya miaka 5 kimepungua kutoka asilimia 44 mwaka 2016 hadi asilimia 35.6 mwaka 2021/2022. Hata hivyo, amesema kuwa kiwango hicho bado kiko juu kitaifa, huku Ruvuma ikishika nafasi ya tano kwa udumavu wa juu.
Dkt. Chomboko amesema malengo ya mkoa ni kupunguza udumavu hadi chini ya asilimia 20 ifikapo mwaka 2030.
Aidha, wadau mbalimbali wa maendeleo ya lishe wameahidi kuendelea kushirikiana na serikali katika kuimarisha mifumo ya lishe, kutekeleza sera, mipango na tafiti zinazoongoza maamuzi sahihi ya uwekezaji katika lishe. Wamesema mshikamano huo ni muhimu katika kukabiliana na changamoto za utapiamlo, hususan udumavu kwa watoto.
Mkurugenzi wa Lishe kutoka Wizara ya Afya, Bi. Neema Joshua, amesisitiza kuwa lishe bora ni msingi wa afya kwa watu wa rika zote na kwamba mabadiliko chanya huanza katika kaya. Amesema juhudi zinazoendelea kufanywa na serikali na wadau zimeanza kuleta matokeo mazuri katika kupunguza matatizo ya lishe nchini.
Maadhimisho hayo yameendelea kuwa jukwaa la kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa lishe bora na kuonesha mchango wa kila mdau katika kuboresha afya na ustawi wa wananchi. Halmashauri ya Madaba imepongezwa kwa kuwa miongoni mwa halmashauri zinazotekeleza kwa vitendo uwekezaji katika lishe kwa manufaa ya wananchi wake.
MADABA - RUVUMA
Anwani ya Posta: 38 BARABARA YA KIFAGURO MAGINGO, P.O.BOX 10, 57186 MADABA, SONGEA
Simu: 0252951052
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@madabadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Madaba.Haki zote zimeifadhiwa