Timu ya ukaguzi kutoka Sekretarieti ya Menejimenti ya Mkoa wa Ruvuma imehitimisha ziara yake ya siku ya pili katika Wilaya ya Madaba kwa kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika Kata ya Gumbiro na maeneo jirani.
Miongoni mwa miradi iliyotembelewa ni Mradi wa ujenzi wa madarasa mawili na vyoo vyenye matundu 12 katika Shule ya Msingi Gumbiro, unaotekelezwa kupitia mpango wa GPE TSP wenye thamani ya shilingi milioni 68.4, ambao kwa sasa umefikia asilimia 96 ya ukamilifu.

Aidha, timu hiyo ilitembelea Kituo cha Afya Gumbiro, ambako unatekelezwa mradi mkubwa wenye thamani ya shilingi milioni 250 unaohusisha ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD), vyoo, shimo la kutupia kondo la nyuma, shimo la taka, mnara wa tanki, pamoja na majengo mengine ya huduma za afya.

Kwa mujibu wa viongozi wa ukaguzi, miradi hiyo inatekelezwa kwa kiwango cha kuridhisha, huku wakisisitiza umuhimu wa kuhakikisha ubora unaozingatia thamani ya fedha na kukamilisha miradi kwa wakati.
Timu hiyo pia ilitembelea Zahanati ya Lutukira, ambapo ilijionea maendeleo ya uboreshaji wa huduma za afya kwa wananchi wa eneo hilo.

Ziara hiyo inalenga kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kubaini changamoto zinazoikabili, na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa lengo la kuboresha huduma kwa wananchi wa Wilaya ya Madaba.

MADABA - RUVUMA
Anwani ya Posta: 38 BARABARA YA KIFAGURO MAGINGO, P.O.BOX 10, 57186 MADABA, SONGEA
Simu: 0252951052
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@madabadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Madaba.Haki zote zimeifadhiwa