Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike yamefanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Madaba, Wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma, yakienda sambamba na kaulimbiu ya mwaka 2025 isemayo “Mimi ni msichana, kinara wa mabadiliko kwa Tanzania tuitakayo 2050.”
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Bi. Mariam Juma, ambaye aliwataka wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuwekeza katika elimu, afya na ustawi wa mtoto wa kike ili kumwezesha kuwa kiongozi wa mabadiliko chanya kwa taifa la kesho.
Bi. Mariam alisema maadhimisho hayo ni sehemu ya kutambua changamoto mbalimbali zinazowakabili watoto wa kike, ikiwemo ukosefu wa elimu bora, mimba za utotoni, ukatili wa kijinsia na ukosefu wa fursa za kiuchumi, hivyo jamii inapaswa kushirikiana kuhakikisha wasichana wanapata haki na nafasi sawa na wavulana.
Sherehe hizo zilipambwa na burudani mbalimbali ikiwemo maigizo, ngonjera, mashairi na maonesho ya mitindo ya mavazi, yaliyobeba jumbe za kumtia moyo mtoto wa kike kuwa jasiri na mwenye ndoto kubwa.
Katika kuunga mkono juhudi za kumjengea mtoto wa kike mazingira salama ya kujifunza, Benki ya NMB ilishiriki kwa kutoa mchango wa taulo za kike, ikiwa ni ishara ya kuthamini na kujali afya ya mtoto wa kike.
Maadhimisho haya hufanyika kila mwaka ifikapo tarehe 11 Oktoba, kufuatia tamko la Umoja wa Mataifa namba 66 la tarehe 19 Desemba 2011, lenye lengo la kutambua na kushughulikia changamoto zinazowakabili watoto wa kike duniani.
MADABA - RUVUMA
Anwani ya Posta: 38 BARABARA YA KIFAGURO MAGINGO, P.O.BOX 10, 57186 MADABA, SONGEA
Simu: 0252951052
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@madabadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Madaba.Haki zote zimeifadhiwa