Mkutano Mkuu wa 32 wa Wajumbe Wawakilishi wa WINO SACCOS umefanyika katika Ukumbi wa WIDA, kijiji cha Lilondo, Wilaya ya Madaba, ambapo umehudhuriwa na viongozi, watendaji na wanachama wa chama hicho cha ushirika.
Akizungumza katika mkutano huo, Afisa Ushirika wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba, Ndugu Sadam Fupi, amewataka viongozi na watendaji wa WINO SACCOS kuendelea kusimamia misingi ya ushirika kwa kuhakikisha huduma bora zinatolewa kwa wanachama na jamii kwa ujumla.
Aidha, Ndugu Fupi amesisitiza umuhimu wa kufuatilia mikopo iliyocheleweshwa kurejeshwa, akibainisha kuwa ucheleweshaji wa marejesho unaathiri maendeleo ya chama na kuleta taswira ya kutowajibika kwa baadhi ya wanachama.
Katika mkutano huo, ilielezwa kuwa Wino SACCOS imepata hati safi kutoka kwa Mkaguzi wa Vyama vya Ushirika, jambo lililopongezwa na wajumbe wote kama ishara ya uwajibikaji na utunzaji mzuri wa mali za chama. Aidha, imeelezwa kuwa jumla ya wanachama 212 wamefikisha hisa zao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya WINO SACCOS, aliwashukuru wajumbe na watendaji wote kwa ushirikiano wao, huku akisisitiza umuhimu wa kuyatekeleza maazimio yote yaliyopitishwa katika mkutano huo kwa pamoja.
Naye mwakilishi kutoka Chuo cha Ushirika Moshi, Ndugu Benitho, aliwataka wanachama kuongeza hisa zao ili kuboresha mtaji wa chama na kujihakikishia uanachama halali. Pia aliwakumbusha kutunza nyaraka zote muhimu za taasisi na aliupongeza mkutano kwa kuwa wa “kisayansi” unaolenga utekelezaji wa maazimio kwa vitendo.



MADABA - RUVUMA
Anwani ya Posta: 38 BARABARA YA KIFAGURO MAGINGO, P.O.BOX 10, 57186 MADABA, SONGEA
Simu: 0252951052
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@madabadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Madaba.Haki zote zimeifadhiwa