MADABA, 18 OKTOBA 2025 – Mkutano Mkuu wa 28 wa Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo Mahanje (MAHANJE SACCOS) umefanyika leo katika Ukumbi wa Amani, ukiwaleta pamoja wanachama, viongozi na wadau wa ushirika kwa lengo la kujadili maendeleo na mikakati ya kuimarisha huduma za kifedha ndani ya chama.
Mkutano huo ulifunguliwa rasmi na Afisa Ushirika wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba, Ndugu Sadam Fupi ambaye alitoa wito kwa wanachama kuendelea kuimarisha ushirika kwa kuweka akiba, kukopa na kununua hisa, ili kukuza mtaji wa chama na kuhakikisha uendelevu wake.
Ndugu Fupi alisema kuwa, maendeleo yanayoonekana ndani ya MAHANJE SACCOS ni ishara kwamba wanachama na viongozi wanafanya kazi kwa bidii na uwajibikaji, akisisitiza kuwa ushirika ni chombo muhimu katika kuinua kipato cha wananchi wa kipato cha chini.
Aidha, aliwataka viongozi wa chama hicho kusimamia shughuli za SACCOS kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za ushirika, huku akihimiza uadilifu na uwazi katika matumizi ya fedha.
Katika mwaka wa 2025, MAHANJE SACCOS imepata mafanikio makubwa ikiwemo Kutoa mikopo kwa wanachama yenye thamani ya TZS Milioni 319.3, Kushinda Tuzo ya SACCOS Bora Tanzania kwa kundi la uwezeshaji wa vijana katika sekta ya kifedha, iliyotolewa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Kushika nafasi ya pili kitaifa kwa SACCOS bora za kijamii Daraja A, Ukaguzi wa hesabu kufikia mwaka 2024 na COASCO, ulioonesha usimamizi mzuri wa fedha pamoja na Ongezeko kubwa la wanachama katika kipindi cha Januari hadi Septemba 2025.
Katika mkutano huo, wanachama walipata fursa ya kupitia taarifa mbalimbali na mapendekezo ya kuboresha huduma za mikopo na uwekaji wa akiba. Pia, baadhi ya wanachama walipewa pongezi na kupatiwa vyeti kwa mchango wao mkubwa katika kukuza hisa na kuhamasisha wengine kushiriki kikamilifu.
Mkutano huo uliendelea kwa mijadala ya ajenda kuu za chama, ikiwemo tathmini ya utendaji wa mwaka uliopita na kupanga mikakati mipya ya kuboresha huduma kwa wanachama, kabla ya kufungwa rasmi na Kamati Kuu ya SACCOS.
MADABA - RUVUMA
Anwani ya Posta: 38 BARABARA YA KIFAGURO MAGINGO, P.O.BOX 10, 57186 MADABA, SONGEA
Simu: 0252951052
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@madabadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Madaba.Haki zote zimeifadhiwa