MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amekanusha taarifa zilizosambaa mtandaoni zikidai katika Halmashauri ya Madaba kuna shule inayoitwa Litapatile ambayo wanafunzi wanasoma kwenye kibanda cha nyasi.
Akizungumza na waandishi wa Habari ofisini kwake Aprili 22 mwaka huu,RC Ibuge amesema video hiyo inaonesha uwepo wa wanafunzi,waliovalishwa sare za shule wakiwa katika kibanda cha miti ambacho msimuliaji anaita shule ikiwa na wanafunzi wanaodaiwa kusoma kuanzia darasa la Awali,kwanza,pili hadi la tatu.
Brigedia Jenerali Ibuge alibainisha Zaidi kuwa video hiyo inasimulia kuwa shule hiyo ina Mwalimu wa kujitolea anayedaiwa kulipwa na wazazi na kwamba wananchi hao wanatamani kusaidiwa kujengewa darasa la kusomea watoto wao.
“Ndugu wanahabari,ukweli ni kwamba hakuna shule inayoitwa Litapatile katika Halmashauri ya Madaba mkoani Ruvuma,chanzo cha taarifa hiyo ni uzushi’’.alisema.
RC Ibuge ametoa rai kwa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma na watanzania kwa ujumla kupuuzia taarifa hiyo ambayo ina malengo binafsi ya kuhalalisha kosa la wazazi la kuwanyima haki ya kusoma watoto wao.
Hata hivyo amesema wananchi wameacha kwa makusudi kuishi katika maeneo rasmi ya vijiji na vitongoji na kuamua kwenda kuishi porini umbali wa kilometa Zaidi ya 50 toka kijijini kwa kisingizio cha kufanya shughuli za uzalishaji mali ambazo ni kilimo na ufugaji.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma ameutaja msimamo wa serikali ni kwamba,watoto hao wanayo haki ya kupata elimu kwa mujibu wa Katiba ya Nchi na kwamba wazazi wao wanawajibu wa kuhakikisha watoto wao wanaandikishwa na kuhudhuria masomo kwa mujibu wa taratibu.
“Pamoja na kuwepo utaratibu wa shule shikizi,bado shule hizo zina utaratibu wake wa kuanzishwa ikiwemo kuwepo na makazi rasmi ,kibanda hiki kipo porini,hakuna hata njia ya kufika huko kwa usafiri isipokuwa kwa miguu,shule shikizi inahitaji huduma za kielimu ili watoto wapate haki ya kupata elimu bora’’,alisisitiza Ibuge.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa ametoa rai kwa wazazi na walezi kuhakikisha kuwa shughuli zao haziathiri haki ya watoto wao kuandikishwa na kupata elimu.
Amesisitiza kuwa serikali ya Mkoa inaendelea kusimamia haki ya watoto kupata elimu kwa kutekeleza Sheria ya Elimu namba 25 ya mwaka 1976 inayolinda haki ya msingi ya watoto wote kupata elimu.
Ametahadharisha kuwa ni kosa kwa mzazi kutohakikisha kuwa mtoto wake anaendelea na shule hadi kufikia darasa la saba na kwamba mtu yeyote atakayesababisha mtoto wake asiendelee na shule atatiwa hatiani.
Amesisitiza kuwa serikali haitamvumilia mzazi yeyote atakayefanya kwa makusudi kumnyima haki ya kupata elimu mtoto wake kwa kisingizio chochote ikiwemo kwenda kuishi porini kwa kisingizio cha kulima au kufuga.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma
Aprili 23,2022
MADABA - RUVUMA
Anwani ya Posta: 38 BARABARA YA KIFAGURO MAGINGO, P.O.BOX 10, 57186 MADABA, SONGEA
Simu: 0252951052
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@madabadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Madaba.Haki zote zimeifadhiwa