Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi wa Jimbo la Madaba, Wakili Abdul M. Manga, ameongoza mafunzo maalum kwa Makarani Waongozaji wa Vituo vya Kupigia Kura yatakayohusika katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025. Mafunzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Madaba Day, yakilenga kuongeza uelewa na uadilifu wa watendaji hao kuelekea uchaguzi huo muhimu wa kitaifa.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Wakili Manga amewataka Makarani hao kufanya kazi kwa uwazi, uadilifu na kutokuegemea upande wowote wa kisiasa, huku wakizingatia misingi ya demokrasia na katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Ni vyema mkatambua kwamba, kwa mujibu wa Ibara ya 74(6) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ndiyo yenye mamlaka ya kusimamia na kuratibu uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani,” alisema Ndg. Manga, akisisitiza wajibu wa kikatiba wa watendaji hao katika kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na wa haki.
Mafunzo hayo pia yaliambatana na viapo vya kutunza Siri na kujitoa uanachama, lakini pia kua na uaminifu na uadilifu, vilivyoapishwa kwa Makarani wote waongozaji wa vituo vya kupigia kura, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuhakikisha zoezi la upigaji kura linaendeshwa kwa weledi.
Jumla ya Makarani kutoka vituo 132 vya kupigia kura vilivyopo katika kata nane za Halmashauri ya Wilaya ya Madaba walihudhuria mafunzo hayo.
Washiriki walipata nafasi ya kuuliza maswali, kutoa maoni na kujadiliana kuhusu mbinu bora za kusimamia uchaguzi. Waliahidi kutekeleza viapo vyao kwa uaminifu ili kuhakikisha wananchi wanapata haki yao ya kikatiba ya kuchagua viongozi wanaowataka kwa amani na utulivu.



MADABA - RUVUMA
Anwani ya Posta: 38 BARABARA YA KIFAGURO MAGINGO, P.O.BOX 10, 57186 MADABA, SONGEA
Simu: 0252951052
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@madabadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Madaba.Haki zote zimeifadhiwa