Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Madaba, Wakili Abdul Manga, amefunga rasmi mafunzo ya siku mbili kwa Wasimamizi wa Vituo na Wasimamizi Wasaidizi wa Vituo vya Kupigia Kura yaliyofanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Madaba.
Akizungumza wakati wa hafla ya kufunga mafunzo hayo, Wakili Manga aliwataka wasimamizi wote kufanya kazi zao kwa uzalendo, uadilifu, ushirikiano na weledi wa hali ya juu, akisisitiza kuwa jukumu walilopewa ni la kizalendo na linahitaji nidhamu na uwajibikaji mkubwa.
“Kazi mnayoenda kufanya ni ya kizalendo na ya kulinda demokrasia ya nchi yetu. Fanyeni kazi kwa weledi, kwa kuzingatia maelekezo, na msikubali kufanya makosa ya uzembe ambayo yanaweza kuharibu mchakato wa uchaguzi,” alisema Wakili Manga.
Miongoni mwa mambo yaliyosisitizwa katika mafunzo hayo ni pamoja na:
Kufanya kazi kwa uzalendo na weledi, wakitambua kuwa uchaguzi ni wa taifa zima.
Kufuata maelekezo ya Msimamizi wa Kituo kama kiongozi mkuu wa kituo husika.
Kuhakiki vifaa vya uchaguzi kwa haraka mara baada ya kuvipokea, na kutoa taarifa mapema iwapo kutakuwa na upungufu.
Kujenga ushirikiano wa timu na kuhakikisha hakuna anayeondoka kituoni bila maelekezo ya msimamizi mkuu.
Kutumia lugha nzuri kwa wapiga kura na kuwapa kipaumbele watu wenye mahitaji maalum.
Aidha, Wakili Manga aliwakumbusha maafisa hao kuwa wamebakisha siku chache kabla ya siku ya uchaguzi, hivyo ni muhimu kutumia muda uliosalia kujisomea kwa kina kitabu cha maelekezo ya wasimamizi ili kuongeza uelewa na kujiamini.
Mafunzo hayo ni sehemu ya maandalizi ya uchaguzi mkuu unatarajiwa kufanyika tarehe 29 Oktoba, 2025, ambapo wananchi wanatarajia kuchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mbunge na Diwani.





MADABA - RUVUMA
Anwani ya Posta: 38 BARABARA YA KIFAGURO MAGINGO, P.O.BOX 10, 57186 MADABA, SONGEA
Simu: 0252951052
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@madabadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Madaba.Haki zote zimeifadhiwa