WANANCHI wa kijiji cha Igawisenga Halmashauri ya Madaba mkoani Ruvuma,wameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuanza kutekeleza mradi mkubwa wa maji unaokwenda kumaliza kero ya maji safi na salama katika kijiji hicho.
Akiongea kwa niaba ya wananchi mbele ya Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge,Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji hicho Paul Ndikweje alisema, kwa muda mrefu hawajawahi kupata maji ya bomba na hivyo kulazimika kutumia maji ya visima vya asili.
Alisema,kujengwa kwa mradi huo ni faraja kubwa kwao na unakwenda kuleta matumaini mapya kwa sababu walishakata tamaa kupata maji ya bomba hasa ikizingatiwa umbali wa kijiji hicho kutoka makao makuu ya wilaya na mkoa.
Aidha,ameomba Wakala wa maji vijijini Ruwasa wilaya ya Songea kuwaunganishia maji kwenye nyumba zao kwani kufanya hivyo itakuwa rahisi kuchangia gharama na kuepusha migogoro, badala ya kujenga vituo vingi vya kuchotea maji(DP).
Alisema, wako tayari kulipia gharama za kuunganishiwa maji kwenye nyumba ambapo baadhi ya wananchi wameshajiandaa kuweka fedha kidogo kidogo na wanachosubiri ni kukamilika kwa mradi huo ambao wanaamini utaharakisha maendeleo.
Meneja wa Ruwasa wilaya ya Songea Mathias Charles alisema, mradi wa maji Igawisenga unatekelezwa kwa kutumia fedha za program ya malipo kwa matokeo na umesanifiwa kuhudumia wananchi 2,275 ifikapo mwaka 2041 ambao kwa sasa wanakadiriwa kuwa 1,336.
Alisema, gharama za utekelezaji wa mradi huo ni Sh.216,831,229.00 ambao unatekelezwa na Ruwasa kwa kutumia wataalam wa ndani na ulianza Mwezi Februari 2021 na umefikia asilimia 80.
Kwa pande wake Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge, ameipongeza Ruwasa kwa kutekeleza mradi huo wa maji ambao utakapo kamilika utamaliza kero ya muda mrefu ya maji safi na salama kwa wananchi wa kijiji cha Igawisenga.
Brigedia Jenerali Ibuge, ameagiza mradi huo ukamilike kama ulivyopangwa na kuitaka Ruwasa kushirikiana na Serikali ya kijiji na wananchi namna ya kuendesha mradi huo na kutunza vyanzo kwani hatua hiyo itasaidia wananchi kuona mradi huo ni wao na kuulinda.
Alisema, maji ni muhimu sana kwa maisha ya Binadamu na maendeleo ya Nchi yetu,hata hivyo hajaridhishwa kuona baadhi ya vyanzo vya maji havijalindwa kikamilifu na hivyo kuleta mashaka makubwa.
Alisema, Rais Samiha Suluhu Hassan amekusudia kwa dhati kumtua ndoo mama kichwani, ndiyo maana anaendelea kutoa fedha za kujenga miradi ya maji, hata hivyo ni lazima wananchi waelimishwe kuhusu madhara ya kulima na kufanya shughuli mbalimbali kwenye vyanzo na hifadhi za maji.
Brigedia Jenerali Ibuge ameitaka Ruwasa na uongozi wa Bonde la Ziwa nyasa ,kuhakikisha wanatumia rasilimali na nguvu kubwa kulinda vyanzo ili visiendelee kuvamiwa na wananchi na kuweka alama ambayo itazuia wananchi kuingia katika maeneo hayo.
Ameigiza Halmashauri ya wilaya Madaba kupitia Baraza la Madiwani, kuendelea kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira na kutunza vyanzo vya maji kwa faida ya sasa na baadaye.
.
MADABA - RUVUMA
Anwani ya Posta: 38 BARABARA YA KIFAGURO MAGINGO, P.O.BOX 10, 57186 MADABA, SONGEA
Simu: 0252951052
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@madabadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Madaba.Haki zote zimeifadhiwa