BENKI ya NMB imetoa msaada wa vifaa vyenye thamani ya shilingi milioni 32 katika wilaya za Namtumbo na Songea mkoani Ruvuma.
Akizungumza kwa nyakati tofauti katika hafla ya ujtoaji wa vifaa hivyo katika shule tatu za msingi zilizopo Manispaa ya Songea,Meneja wa NMB Kanda ya Kusini Janeth Shango amezitaja shule zilizopata vifaa hivyo kuwa ni shule ya msingi Legele iliyopata mabati 60 kwa ajili ya kuezeka darasa la kwanza na choo.
Shule nyingine ni Mshanganokati iliyopewa madawati 80 na shule ya msingi Chandamali ambayo imepewa meza 21,viti 21 na kabati nne ambapo amesisitiza kuwa Benki ya NMB imeamua kushirikiana na jamii kwa kutoa msaada katika shule hizo tatu .
Katika Wilaya ya Songea Halmashauri ya Madaba,Meneja huyo wa Kanda amesema NMB imetoa vitanda 25 katika shule ya sekondari Gumbiro,viti na meza 50 katika shule ya sekondari Nguluma vifaa vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni kumi.
Kwa mujibu wa Meneja huyo,Benki ya NMB katika wilaya ya Namtumbo imetoa msaada wa vifaa mbalimbali kwa ajili ya hospitali ya wilaya ya Namtumbo vyenye thamani ya shilingi milioni kumi.
Shango amevitaja vifaa hivyo kuwa ni vitanda vitano vya wagonjwa na godoro zake,vitanda viwili vya kisasa vitakavyotumika wakati wa kujifungua akinamama na mashuka 25 kwa ajili ya vitanda hivyo.
“Kwa miaka kadhaa sasa NMB imekuwa ikisaidia miradi mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi kwa kujikita zaidi kwenye miradi ya elimu kwa kutoa madawati na vifaa vya kuezekea na kwenye afya kwa kutoa vitanda na magodoro yake’’,alisema.
Amesisitiza kuwa kupitia jamii,NMB inatambua kuwa wanapatikana wateja wake wengi,kwa hiyo kurudisha sehemu ya faida kwa jamii ni utamaduni wa Benki hiyo ambayo imezifikia wilaya zote nchini kwa asilimia 100.
Akizungumza katika hafla ya kugawa vifaa vya hospitali ya Namtumbo,mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Sophia Kizigo ameishukuru Benki ya NMB kwa msaada huo ambao amesema umeongeza vitanda katika hospitali hiyo ambayo imeanza kulaza wagonjwa na kwamba kabla ya msaada huo hospitali ilikuwa na vitanda kumi tu.
“Tuliamua kuanzia mwaka jana kuanza kulaza wagonjwa,hivyo tulianza na vitanda kumi,leo NMB wametuletea vifaa vya milioni kumi kwa ajili ya kusaidia hospitali yetu,tunawashukuru sana’’,alisisitiza Kizigo.
Kwa upande wake Meneja wa NMB Tawi la Songea David Zake akizungumza kwa nyakati tofauti katika zoezi la utoaji vifaa katika Manispaa ya Songea,amesema Benki ya NMB ni sikivu kwa sababu imekuwa inarudisha mapato yake ya asilimia moja kwa jamii kila mwaka .
Amesema hali hiyo ndiyo iliyosababisha shule tatu za msingi kuwa miongoni mwa shule ambazo zimepata mchango mkubwa kutoka NMB.
Mgeni rasmi katika hafla ya utoaji madawati hayo Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Songea Pendo Ndumbaro amesema NMB imekuwa karibu kwa jamii wilayani Songea kwa kutoa misaada mbalimbali katika shule na vituo vya afya ambapo amesema, Benki hiyo inaunga mkono jitihada za serikali kusaidia wananchi.
Naye Afisa Elimu Msingi Manispaa ya Songea Zakia Fandey amesema msaada huo utaongeza mahudhurio mazuri ya wanafunzi hasa katika shule msingi Mshanganokati iliyokuwa na uhaba mkubwa wa madawati na kwamba ufundishaji na ujifunzaji utaimarika .
Mkuu wa shule ya sekondari Gumbiro Jofrey Lyosi akizungumza baada yak kupokea msaada wa vitanda 25 kwa ajili ya kulala wanafunzi,amesema wanafunzi hao tangu mwaka 2012 wamekuwa wanalala chini kwenye magodoro bila kuwa na vitanda hivyo NMB ime,kuwa ukombozi kwa wanafunzi hao.
Benki ya NMB katika nchi nzima ina matawi 225,mashine za kutolea fedha ATM zaidi ya 800,wakala zaidi ya 6,000 na idadi ya wateja zaidi ya milioni tatu.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Machi 14,2021
MADABA - RUVUMA
Anwani ya Posta: 38 BARABARA YA KIFAGURO MAGINGO, P.O.BOX 10, 57186 MADABA, SONGEA
Simu: 0252951052
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@madabadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Madaba.Haki zote zimeifadhiwa