Mkoa wa Ruvuma umefanikiwa kuwapangia shule za sekondari watoto wote 27,135 waliofaulu mtihani wa kuhitimu darasa la saba mwaka 2020.
Akizungumza kwenye kikao cha kutangaza wanafunzi waliochaguliwa kuanza kidato cha kwanza mwaka 2021,kilichofanyika ukumbi wa Manispaa ya Songea,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amesema Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa tisa nchini iliyofanikiwa kuwapangia shule watoto wote waliofaulu.
Mndeme amesema kati ya wanafunzi waliofaulu wavulana ni 12,799 na wasichana ni 14,336 na kwamba ufaulu huo ni sawa na asilimia 78.50 ya wanafunzi waliohitimu mwaka 2020.
Hata hivyo amesema mwaka 2019 ufaulu wa darasa la saba ulikuwa ni asilimia 83.70 hivyo mwaka huu ufaulu umeshuka kwa asilimia 5.2 ambapo mwaka jana wanafunzi waliofaulu walikuwa 32,298 kati yao wavulana 15,236 na wasichana 17,062.
“Tuhakikishe kuwa watoto wote waliofaulu wanaripoti shule mara baada ya shule kufunguliwa Januari 2021 na wazazi watakaokiuka maelekezo haya wachukuliwe hatua,isiwepo sababu yoyote itakayomzua mwanafunzi aliyefaulu kuanza shule’’,alisisitiza Mndeme.
Mndeme pia amepiga marufuku michango ya shule inayokwenda kinyume na maelekezo yaliyotolewa na serikali kupitia waraka wa Elimu bila ada.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa amewapongeza viongozi na watendaji wote wa serikali kwa kufanya elimu kuwa kipaumbele cha kwanza kwa kuhakikisha kuwa miundombinu ya shule inajengwa.
“Ninaagiza mwakani kusiwepo na upungufu hata wa chumba kimoja cha darasa na samani zake,pia nazipongeza Halmashauri za Madaba na Manispaa ya Songea kuwa na ziada ya jumla ya madarasa 21’’,alisema Mndeme.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma Stephen Ndaki amewaagiza maafisa elimu na wadau wote wa elimu kusimamia taaluma ili ufaulu uweze kuongezeka na kuufanya Mkoa wa Ruvuma kuwa na ufaulu wa juu.
Amezipongeza kamati za mitihani katika shule kwa kufanyakazi kubwa mwaka huu,hata hivyo ameshangazwa katika kipindi cha mitihani baadhi ya walimu na wanafunzi wao wanashindwa kujiamini.
Ndaki amesema katika utafiti mdogo uliofanyika umebaini sehemu kubwa ya wasimamizi wa taaluma shuleni hawafanyakazi yao kikamilifu ya kusimamia walimu ili waweze kutoka na matokeo mazuri.
“Ukiangalia matokeo ya mwaka 2020 utabaini kuwa ni wanafunzi wachache waliofikia ufaulu wa daraja A,wengi wanapata C na B alama ambazo haziwezi kuwafanya watoto wetu waweze kushindana kwenda kwenye shule za bweni nje ya Mkoa wa Ruvuma’’,alisema Ndaki.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Desemba 18,2020
MADABA - RUVUMA
Anwani ya Posta: 38 BARABARA YA KIFAGURO MAGINGO, P.O.BOX 10, 57186 MADABA, SONGEA
Simu: 0252951052
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@madabadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Madaba.Haki zote zimeifadhiwa