WAKALA wa barabara za vijijini na mijini(Tarura)imekamilisha ujenzi wa daraja lililojengwa kwa teknolojia ya mawe katika mto Mgombezi linalounganisha kijiji cha Lipupuma,Mgombezi na Chechengu katika Halmashauri ya Madaba wilayani Songea.
Meneja wa TARURA Wilaya ya Songea Bakari John alisema,daraja la mto Mgombezi lina urefu wa kilomita 41 na ujenzi kwa kutumia teknolojia ya mawe ni wa gharama nafuu na la kwanza kujengwa wilayani Songea.
Alitaja gharama za ujenzi wa daraja hilo ni shilingi milioni 152 tu na kueleza kuwa, kama wangejenga kwa kutumia zege na chuma kama ilivyo kwa madaraja mengine basi serikali ingetumia zaidi ya shilingi milioni 500.
Alisema,kabla ya ujenzi wa daraja hilo wananchi walilazimika kupita kwenye daraja la miti lililojengwa na wananchi wenyewe,hata hivyo wakati wa masika halikuwasaidia kutokana na mto Mgombezi kujaa maji mengi na kukatisha mawasiliano kati ya upande mmoja na mwingine.
Alieleza kuwa, kujengwa kwa daraja hilo ni ukombozi mkubwa kwa wananchi wa maeneo hayo kwani limetatua kero ya muda mrefu ya usafiri na usafirishaji wa mazao hasa mbao na Tangawizi.
Meneja huyo wa Tarura aliongeza kuwa, kazi iliyobaki ni kuendelea kufungua barabara za kuunganisha mashamba ili kuwawezesha wananchi kuendelea na shughuli zao za kilimo kwa urahisi.
Baadhi ya wananchi waliokutwa wakivuka katika daraja hilo,wameishukuru serikali kwa uamuzi wake wa kujenga daraja la kudumu kwani kwa muda mrefu walikuwa wakiteseka kupita kwenye maji pindi wanapohitaji kuvuka upande mmoja kwenda mwingine.
Nuru Francis mkazi wa Lipupuma alisema,walikuwa na hali mbaya kwani walilazimika kupita kwenye mto huo wenye maji mengi kila siku na wakati wa masika walishindwa kwenda kwenye shughuli zao za uzalishaji mali kutokana na mto huo kujaa maji.
Michael Brumo,ameipongeza serikali ya awamu ya sita kuona umuhimu wa kujenga daraja katika eneo hilo kwa sababu ilikuwa changamoto kubwa kila wanapotakakusafirisha mazao yao kutoka shambani kwenda sokoni.
Robert Mbilinyi,ameishauri serikali kuendelea kujenga madaraja kwa kutumia teknolojia ya mawe ambayo ni ya gharama nafuu na kuachana na ujenzi wa madaraja ya chuma ambayo wakati mwingine baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu wanahujumu kwa kuiba vyuma na hivyo kuisababishia serikai hasara kubwa.
MADABA - RUVUMA
Anwani ya Posta: 38 BARABARA YA KIFAGURO MAGINGO, P.O.BOX 10, 57186 MADABA, SONGEA
Simu: 0252951052
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@madabadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Madaba.Haki zote zimeifadhiwa