MKUU wa mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amesema,hayuko tayari kuona wala kupokea miradi ya barabara na miradi mingine ya maendeleo inayotekelezwa katika mkoa huo iliyojengwa chini ya viwango.
Kanal Laban amesema hayo leo, wakati wa hafla ya usainishaji mikataba 13 ya ujenzi wa miundombinu ya barabara,madaraja na makalavati kati ya Wakala wa barabara za mjini na vijijini(TARURA)mkoa wa Ruvuma na wakandarasi yenye thamani ya Sh.bilioni 6,128,065,525.00 inayokwenda kutekelezwa katika mkoa huo.
Wakandarasi hao wakiongozwa na kampuni ya Ovans Contruction Ltd, wanakwenda kujenga barabara kwa kiwango cha lami, changarawe,madaraja na makalavati katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Ruvuma.
Kanali Laban alisema,fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo zimeshatengwa, na kuwataka wakandarasi kwenda kufanya kazi walizopewa kwa wakati kabla ya mvua za masika hazijaanza kunyesha ili kuepuka changamoto zinazoweza kujitokeza.
“leo wakandarasi mmesaini mikataba mbele yangu,fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara zipo,hakikisheni mnakwenda kujenga barabara za viwango na mnakamilisha kazi kwa muda uliopangwa kama mikataba yenu inavyosema,TARURA sitaki kusikia mnaongeza muda wa ujenzi kwa mkandarasi”alisisitiza Kanal Laban.
Alisema,wananchi wa mkoa wa Ruvuma wanataka barabara zenye viwango zitakazodumu kwa miaka mingi na siyo ndani ya mwaka mmoja zinaanza kufanyiwa matengenezo
Mkuu wa mkoa,amewapongeza wakandarasi walioshinda zabuni hizo na kuwataka kwenda kutekeleza miradi hiyo kwa kuzingatia ubora na muda uliopangwa kwani zikiboreshwa zitachochea ukuaji uchumi wa wananchi na kuboresha sekta ya kilimo ambayo ni uti wa mgongo wa wananchi wa mkoa huo.
Aidha amesisitiza kuwa, mkandarasi atakayejenga barabara na miradi mingine ya maendeleo chini ya kiwango atashughulikiwa na hatopata kazi yoyote katika mkoa wa Ruvuma.
“ninyi ni wakandarasi wazawa,nawaombeni sana kafanyeni kazi zenu kwa ufanisi mkubwa na mshindane na wakandarasi wa nje,Ruvuma tunahitaji barabara nzuri na zenye viwango zitakazo chochea kukua kwa uchumi wa wananchi na mkoa wetu”alisema.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho amesema,amefurahishwa sana kuona wakandarasi wazawa wakiendelea kuaminika,kupata na kufanya kazi za ujenzi wa barabara na miradi mbalimbali.
Alisema,barabara zinazokwenda kujengwa katika maeneo mbalimbali zitakuwa chachu ya maendeleo na kuwa kiungo muhimu cha ukuaji wa uchumi wa mkoa wa Ruvuma,na Chama cha Mapinduzi kina imani kubwa na wakandarasi hao watatimiza wajibu wao.
Mwenyekiti huyo wa Chama cha Mapinduzi, amewaasa wakandarasi walioshinda zabuni hizo kwenda kutekeleza miradi hiyo kwa ufanisi huku akiwataka TARURA kuwa makini kusimamia ujenzi wa barabara hizo kwa hatua zote za utekelezaji wake.
Naye Meneja wa TARURA mkoa wa Ruvuma Mhandisi Wahabu Nyamzungu amesema, Tarura imeingia mikataba 40 na Wakandarasi katika hatua ya kwanza yenye jumla ya Sh.bilioni 13,173,296,710.00 kwa ajili ya kutekeleza kazi mbalimbali za matengenezo ya barabara,ujenzi wa madaraja na makalavati kwa mfuko wa fedha wa barabara,jimbo na tozo.
Alisema,hadi kufikia mwezi Septemba 2022 miradi yote 40 inaendelea kutekelezwa na ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji wake, na katika bajeti iliyotengwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ni Sh.bilioni 6,128,065,525.00.
Alisema,mikataba iliyosainiwa katika awamu ya pili (Phase 11) kati ya TARURA na Wakandarasi ni asilimia 40 na itahusisha ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami changarawe,madaraja na makalavati katika mkoa wote wa Ruvuma.
Amefafanua kuwa, mikataba hiyo inahusisha mikataba mitano ya jimbo inayogharimu Sh.bilioni 2,481,325,500.00,mikataba sita ya tozo yenye thamani ya Sh.bilioni 2,639,562,475.00,mkataba mmoja wa matengenezo kupitia mfuko wa barabara utakaogharimu kiasi cha Sh. milioni 294,903,000.00.
Ameongeza kuwa,mkataba mmoja ni wa fedha maalum kutoka Serikali kuu utakaogharimu jumla ya Sh.milioni 712,274,500.00 ambao utekelezaji wake umeanza mwezi Oktoba 2022 na utamalizika mwezi Februari 2023.
MADABA - RUVUMA
Anwani ya Posta: 38 BARABARA YA KIFAGURO MAGINGO, P.O.BOX 10, 57186 MADABA, SONGEA
Simu: 0252951052
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@madabadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Madaba.Haki zote zimeifadhiwa