RC IBUGE;WATAALAMU WA AFYA TOENI ELIMU ENDELEVU YA KUJIKINGA NA CORONA KWA WANANCHI
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge ameziagiza Halmashauri zote nane kupitia wataalam wa afya kusimamia kutoa elimu ya kujikinga na maambukizi ya wimbi la tatu la corona.
RC Ibuge ametoa maagizo hayo wakati anazungumza na wakuu wa wilaya,wakurugenzi wa Halmashauri na watumishi wa umma ngazi ya Mkoa na wilaya zote kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea.
Amesisitiza elimu endelevu ya kujikinga kabla ya kuugua corona itolewe kwa wananchi ikiwemo kuvaa barakoa,matumizi ya kunawa kwa sabuni na maji titirika na kuepuka mikusanyiko isiyokuwa ya lazima.
“Nimepita na kuzunguka baadhi ya maeneo mjini Songea,nimeona wananchi wameacha zile hatua ambazo tulikuwa tumezichukua katika wimbi la kwanza mfano,nje ya maeneo ya huduma,ndoo hazina maji wala sabuni,tukasimamie kuwaelimisha wananchi kwa sababu kujikinga ni gharama ndogo kuliko kutibu’’,alisisitiza RC Ibuge.
Amesisitiza kuwa corona ipo nchini,ingawa amebainisha kuwa katika Mkoa wa Ruvuma tishio la corona sio kubwa,hata hivyo amesema hakuna mipaka iliyofungwa hivyo kuna mwingiliano mkubwa wa watu kusafiri na kuingia ndani ya Mkoa wa Ruvuma hivyo elimu endelevu ya kujikinga na corona isimamiwe ipasavyo kwa wananchi.
“Suala la kujikinga ni rahisi kuonekana halina umuhimu kama madhara bado hatujayaona,sote tumekuwa tukisikia maelekezo mbalimbali kutoka Wizara ya Afya na kupitia viongozi wa kitaifa akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,wimbi la tatu la corona tayari lipo nchini tuchukue tahadhari’’,alisema RC Ibuge.
Takwimu kutoka Wizara ya Afya zinaonesha kuwa hadi sasa Tanzania ina wagonjwa wa corona 408 waliothibitika kutoka baadhi ya mikoa hapa nchini.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
MADABA - RUVUMA
Anwani ya Posta: 38 BARABARA YA KIFAGURO MAGINGO, P.O.BOX 10, 57186 MADABA, SONGEA
Simu: 0252951052
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@madabadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Madaba.Haki zote zimeifadhiwa