Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amewaagiza maafisa wa ardhi kutatua migogoro ya ardhi kwa kuwatembelea wananchi katika maeneo yao badala ya kusubiri migogoro hiyo kuwakuta maofisini.
RC Ibuge ametoa maagizo hayo wakati anazungumza katika kikao kazi cha watumishi wa sekta ya ardhi mkoani Ruvuma ambacho kimeshirikisha watendaji mbalimbali wakiwemo wakuu wa Wilaya,wakurugenzi wa Halmashauri,makatibu Tawala wa wilaya na watumishi wengine ngazi ya wilaya na Mkoa kilichofanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea.
Maelekezo mengine ambayo ameyatoa RC Ibuge kwa maafisa ardhi ni kuhakikisha wanafanyakazi kwa weledi na kwa kuzingatia maadili ya kazi,kutojiuhusisha kuomba na kupokea rushwa na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu sheria mbalimbali za ardhi.
“Ikumbukwe kuwa baadhi ya migogoro ya ardhi hutokea kutokana na wananchi kutofahamu sheria za ardhi,kwa hiyo kinachohitajika hapa ni uelewa wa sheria ili wananchi kuzifahamu’’,alisisitiza Ibuge.
Brigedia Jenerali Ibuge pia ameagiza kuendelea na ukamilishaji wa kazi zote za urasimishaji wa makazi holela katika Halmashauri zote za Mkoa wa Ruvuma na kwamba kipaumbele kiwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea ambapo zoezi hilo linafanyika kwa kasi ndogo ukilinganisha na wingi wa maeneo yaliyojengwa kiholela.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa ametoa rai kwa wananchi ambao maeneo yao yamechukuliwa kwa ajili ya uwekezaji na yanahitaji fidia kuendelea kuwa watulivu wakati serikali inatafuta fedha kwa ajili ya fidia.Maeneo yanayohitaji fidia yaliyopo Manispaa ya Songea ni Bonde la Mto Ruhila,eneo la EPZA Kata ya Mwengemshindo na barabara ya By Pass ya Mtwara Corridor.
Katika kikao kazi hicho RC Ibuge amewaagiza wanasheria wa Halmashauri zote kwa kushirikiana na maafisa Ardhi na TAKUKURU kutoa elimu ya namna bora ya kufany usuluhisho wa migogoro ya ardhi kwa wajumbe wa Mabaraza ya Ardhi ya Kata kwa sababu wameonekana kuwa sehemu ya kikwazo katika kutenda haki kwa wananchi.
Akizungumza kwenye kikao hicho,Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Mgema ameshauri ili kutatua changamoto za ardhi,bajeti ya kupima ardhi iongezwe ili eneo kubwa la ardhi lipimwe kuepusha migogoro ambayo inatokana na maeneo mengi kutopimwa.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Julai 13,2021
MADABA - RUVUMA
Anwani ya Posta: 38 BARABARA YA KIFAGURO MAGINGO, P.O.BOX 10, 57186 MADABA, SONGEA
Simu: 0252951052
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@madabadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Madaba.Haki zote zimeifadhiwa