WATAALAM zaidi ya 280 kutoka ngazi za Halmashauri na mikoa ya Ruvuma,Njombe na Iringa wamepata mafunzo elekezi ya timu za utekelezaji wa mradi wa Kuimarisha Ujifunzaji katika Elimu ya Awali na Msingi (BOOST) unaogharimu sh.trilioni 1.15 wenye lengo la kujenga madarasa 12,000 na shule salama 6,000 katika nchi nzima.
Mafunzo hayo ambayo yameandaliwa na Ofisi ya Rais TAMISEMI yamefanyika kwa siku mbili katika shule ya sekondari Lugalo Manispaa ya Iringa.
Akizungumza wakati anafungua mafunzo hayo,Mratibu wa Mafunzo kutoka Idara ya Usimamizi wa Elimu Ofisi ya Rais TAMISEMI Yusuph Singo amesema TAMISEMI imeandaa mafunzo hayo katika Kanda tisa kwa lengo la kuwajengea uwezo wajumbe wa timu hizo kuhusu usimamizi wa mradi wa BOOST.
Amezitaja timu hizo kuwa zinaundwa na wajumbe 12 kutoka ngazi ya Halmashauri ambao ni Afisa Elimu Msingi,Afisa Maendeleo ya Jamii,Mhandisi,Mwalimu Mkuu,Afisa Manunuzi,Mthibiti Ubora wa Shule, Afisa Ustawi wa Jamii,Afisa Elimu Kata,Afisa Mipango,Afisa Habari na Mratibu wa Mradi.
Amesema katika ngazi ya Mkoa timu inaundwa na wajumbe wanane ambao ni Afisa Elimu Mkoa,Mratibu wa Mradi wa BOOST,Mhandisi,Afisa Habari,Afisa Maendeleo ya Jamii,Afisa Ustawi wa Jamii,Afisa Mipango na Mdhibiti Ubora wa Shule Kanda.
“Mheshimiwa Rais ametafuta fedha kiasi cha shilingi Trilioni 1.15 kwa ajili ya uboreshaji mkubwa wa elimu kupitia Mradi wa kuimarisha ujifunzaji shule za msingi na awali, utekelezaji wa mradi huu ni wa miaka mitano utaboresha mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji, ujuzi na ubora wa walimu katika ufundishaji’’,alisisitiza Singo.Baadhi ya washiriki wa mafunzo elekezi ya Timu za utekelezaji wa mradi wa BOOST kutoka mikoa ya Ruvuma,Iringa na Njombe wakiwa kwenye mafunzo katika shule ya sekondari Lugalo Manispaa ya Iringa
Amesema mradi utatekelezwa katika afua mbalimbali ikiwemo kuboresha miundombinu ya shule za msingi kwa kuzingatia mahitaji hususan ujenzi wa madarasa, uimarishaji wa mpango wa shule salama, kuimarisha uwiano wa uandikishwaji wa wanafunzi wa elimu ya awali, kuboresha vifaa na njia za ufundishaji elimu ya awali, pamoja na kuimarisha na kuendeleza mpango wa mafunzo ya walimu kazini.
Mratibu huyo wa Mafunzo wa TAMISEMI amesema katika kipindi cha miaka mitano madarasa 12,000 yatajengwa nchi nzima katika shule za msingi kupitia mradi wa BOOST na kwamba kwa kila mwaka yanatarajiwa kujengwa madarasa 3,000 ambapo afua zote zitatekelezwa kwa utaratibu wa lipa kulingana na matokeo(EP4R).
Hata hivyo amesema kupitia mradi wa BOOST shule za msingi 800 zinatarajiwa kuwekewa vifaa vya TEHAMA ili kuwawezesha walimu kujifunza utoaji wa elimu endelevu hivyo kuboresha elimu ya msingi.
Kwa upande wake Mratibu wa Mpango wa Shule Salama kitaifa Hilda Mgomapayo amesema kupitia mradi wa BOOST shule salama 6,000 zinatarajiwa kujengwa katika nchi nzima katika kipindi cha miaka mitano ya utekelezaji wa mradi huu ambapo katika awamu ya kwanza zinatarajiwa kujengwa shule 1000.
Amesema shule salama zitawajengea uwezo wanafunzi kujiamini katika mfumo wa elimu,kuimarisha stadi za Maisha,mawasiliano na mahusiano hivyo Watoto kufikia malengo yao.
Kwa upande wake Mwezeshaji kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Lugalata Mwshemi akizungumzia afua ya kuongeza uandikishaji Watoto wa awali,amesema kupitia mradi wa BOOST inatarajiwa kuboresha, uandikisha wa wanafunzi elimu ya awali kwa kuongeza idadi ya wanafunzi katika kipindi cha miaka mitano ya utekelezaji.
Amesema katika utekelezaji wa mwaka wa kwanza uandikishaji wa elimu ya awali 2021/2022 unatarajiwa kuwa ni asilimia 75,mwaka 2022/2023 asilimia 80.14,mwaka 2023/204 asilimia 81.76,mwaka 2024/2025 asilimia 83.38 na mwaka 2025/2026 kuwa asilimia 85.
Hata hivyo amesema lengo ni kuhamasisha jamii kuhusu uandikishaji wanafunzi wa awali wenye umri wa kati ya miaka mitatu hadi mitano na kuhakikisha wanafunzi wote waliondikishwa wanakamilisha mafunzo kwa mwaka mmoja.
Takwimu zinaonesha kuwa hapa nchini kuna shule za msingi zaidi ya 17,000,hata hivyo kupitia mradi wa Kuimarisha Ujifunzaji katika Elimu ya Awali na Msingi (BOOST) watoto zaidi ya milioni 12 wanatarajia kunufaika na mradi huo.
MADABA - RUVUMA
Anwani ya Posta: 38 BARABARA YA KIFAGURO MAGINGO, P.O.BOX 10, 57186 MADABA, SONGEA
Simu: 0252951052
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@madabadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Madaba.Haki zote zimeifadhiwa