MKOA wa Ruvuma umetenga jumla ya ekari 48,343.35 za ardhi kwa ajili ya kilimo cha pamoja na Mkataba kwa zao la Alizeti,Ufuta na Soya ikiwa ni mkakati wake wa kutaka kujitosheleza kwa mafuta ya kula.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amesema hayo jana,wakati akifungua Mkutano wa wadau wa kilimo uliohudhuriwa na Wakuu wa wilaya,Wakurugenzi wa Halmashauri,maafisa ugani na taasisi za fedha.
Aidha amesema, mkakati huo unakusudia na utasaidia Taifa kuepuka kutumia fedha nyingi kuagiza bidhaa hiyo nje ya nchi na kuinua vipato vya wakulima na Nchi kwa jumla.
Ameishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kutenga Sh.bilioni 2.2 kwa ajili ya ununuzi wa mbegu bora za Alizeti ambazo awali zilikuwa zikiuzwa na wafanyabiashara kwa bei ya Sh.35,000 kwa kilo.
Ibuge amesema,kupitia mpango huo sasa mbegu za alizeti zitauzwa kwa bei ya Sh.3,500 kupitia wakala wa mbegu(Asa) sawa na asilimia kumi ya bei ya awali na kuwasihi wananchi wa mkoa wa Ruvuma kutumia fursa hiyo kuwekeza katika kilimo cha zao hilo.
Amesema,katika mkoa wa Ruvuma mahitaji ya mbegu za alizeti,soya na ufuta ni kilo 310,222 na mbolea ni tani 1,662 ambapo kwa msimu wa kilimo 2021/2022 Halmashauri za mkoa huo zimepanga kulima ekari 12,570 kati ya ekari 48,343 zilizotengwa.
Amesema, ekari hizo zitahitaji tani 112 ambapo zao la ufuta mahitaji ni tani 21,soya tani 77 na alizeti tani 14,na kuzielekeza Halmashauri kuhakikisha zinawezesha upatikanaji wa mbegu na pembejeo hizo kwa wakati ili wakulima wasikwame.
Pia amesema, katika msimu wa kilimo 2021/2022 mkoa huo umejipanga kutekeleza mfumo wa kilimo cha pamoja na kilimo cha mkataba(Block Farming& Contract Farming) kwenye Halmshauri ambacho kinahusisha utengaji wa maeneo kwa wakulima hulima eneo moja.
Amesema, kilimo hicho wakulima watapata huduma za ugani na urahisi wa upatikanaji wa pembejeo na masoko ambapo wahusika wa mpango huo ni Vyama vya Ushirika,wakulima,vikundi,taasisi mbalimbali za umma na binafsi na makampuni ya ndani nan je ya Nchi.
Kwa mujibu wa Jenerali Ibuge,Serikali ya mkoa imeridhia kilimo hicho cha mktaba kwa wakulima kinachohusisha makubaliano baini ya mkulima na kampuni au mtoa huduma ambaye atahusika kutoa pembajeo,huduma ya ugani na ununuzi wa mazao kwa lengo la kuinua kipato.
Katika kikao hicho, Ibuge ameziagiza Halmashauri kwenda kuviwezesha vikundi vitakavyohitaji kuwekeza katika mazao hayo, na kuhakikisha wanatenga eneo angalau moja kwa ajili ya taasisi ya utafiti wa kilimo(Tari) ambalo litatumika kama shamba darasa na kuzalisha mbegu bora kwa mazao ambayo Halmashauri itaanza nayo.
Kwa upande wake Katibu Tawala msaidizi uchumi na uzalishaji Jeremiha Sendoro amesema, manufaa ya kilimo cha pamoja ni kutumia rasilimali kidogo kama maafisa ugani wachache kuwafikia wakulima wengi na kalenda ya kuhudumia shamba huandaliwa kwa pamoja.
Sendoro ametaja faida nyingine, ni usambazaji wa pembejeo hufanywa kwa urahisi kwa kuwa mashamba yote yapo kwenye uelekeo mmoja na upatikanaji wa masoko ni rahisi kwa sababu mazao ukusanywa kwenye maghala au soko moja.
MADABA - RUVUMA
Anwani ya Posta: 38 BARABARA YA KIFAGURO MAGINGO, P.O.BOX 10, 57186 MADABA, SONGEA
Simu: 0252951052
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@madabadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Madaba.Haki zote zimeifadhiwa