MKOA wa Ruvuma umeridhia kupandisha hadhi Hifadhi mbili za misitu kuwa mapori ya akiba (Game Reserve) kwa lengo la kuboresha sekta ya utalii kusini.
Mshauri wa Maliasili na Utalii Mkoa wa Ruvuma Afrikanus Challe ameyataja mapori hayo kuwa ni Gesimasowa lenye ukubwa wa kilometa za mraba 764 lililopo Halmashauri ya Madaba wilayani Songea na pori la Litumbandyosi lenye ukubwa wa kilometa za mraba 494 lililopo wilayani Mbinga.
“Mapori yote mawili ni sehemu ya ekolojia ya ushoroba wa Selous-Niassa,hata hivyo hadi sasa bado hifadhi hizo haziajapata Tangazo rasmi la serikali la kuwa ni mapori ya akiba,ingawa mchakato wa kutangaza upo katika hatua za mwisho’’,alisisitiza.
Challe amesema Mkoa wa Ruvuma,una mpango wa kuanzisha mashamba ya wanyapori katika Jumuiya zote tano za uhifadhi,kikiwemo kisiwa cha Lundo ndani ya ziwa Nyasa na katika chuo cha Maliasili cha Likuyusekamaganga wilayani Namtumbo ili wananchi wajifunze na kuanzisha mashamba binafsi ya wanyamapori.
Akizungumzia fursa za utalii zilizopo katika Mkoa wa Ruvuma,amesema Mkoa una fursa za utalii wa kiutamaduni na kiikolojia ambapo amezitaja baadhi ya fursa hizo kuwa ni mapori ya akiba ya Selous,Mwambesi,ziwa Nyasa lenye samaki wa mapambo,visiwa,fukwe za kuvutia na vuvutio vingine lukuki.
Fursa nyingine amezitaja kuwa ni mto Ruvuma wenye maporomoko ya Nakatuta,Tulila na Sunda ambayo yamekuwa yanavutia watalii wengi wa ndani na nje ya nchi.
Challe amezitaja fursa za utalii wa kiutamaduni kuwa ni majengo ya kihistoria yakiwemo makanisa makongwe ya Peramiho,Lituhi na Lundu, makumbusho ya vita ya Majimaji,historia ya machifu wa kiyao,wangoni na historia ya biashara ya utumwa.
Fursa nyingine za utalii wa kiutamaduni amezitaja kuwa ni historia ya wapigania uhuru wa Afrika,jiwe la Mbuji,mapango ya wamatengo na pango la mlima Chandamali ambalo lilikuwa maficho ya Nduna Songea Mbano wakati wa Vita ya Majimaji.
Ili kuhakikisha vivutio vilivyopo vinaleta tija,Challe amesema Mkoa umeendelea kufanya jitihada za kuboresha miundombinu na matangazo katika vyombo vya habari ambayo yatawezesha fursa hizo kufahamika kitaifa na kimataifa.Ameipongeza serikali kuu kwa kuboresha miundombinu ya barabara na anga hivyo kuvutia watalii na kuufungua Mkoa na ukanda wa kusini katika sekta ya utalii na uwekezaji.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari wa Mkoa wa Ruvuma
Juni 9,2021
MADABA - RUVUMA
Anwani ya Posta: 38 BARABARA YA KIFAGURO MAGINGO, P.O.BOX 10, 57186 MADABA, SONGEA
Simu: 0252951052
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@madabadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Madaba.Haki zote zimeifadhiwa