MKOA wa Ruvuma umelenga kupanda miti ya biashara katika eneo lenye ukubwa wa hekta 40,000 hadi kufikia mwaka 2025.
Mshauri wa Maliasili na Utalii wa Mkoa wa Ruvuma Afrikanus Challe amesema mradi huo unatekelezwa kwa miaka kumi kuanzia mwaka 2015,unatekelezwa kwa kupanda miti maeneo ya serikali kuu,serikali za mitaa,vyuo,shule na vijiji.
Challe ameitaja aina ya miti inayopandwa ni ile ambayo inafaa kwa ajili ya malighafi za viwanda vya mazao ya misitu ambayo ni misindano (pine),milingoti(Eucalyptus) na misaji(Teak).
‘Hadi kufikia mwaka 2020 jumla ya miti ya biashara iliyopandwa na wakala wa Huduma za misitu Tanzania(TFS) ni msitu wa hekta 4785,Halmashauri zilipanda miti hekta 425,vyuo na shule hekta 420 na watu binafsi hekta 23,964.
Amesema jumla ya mashamba yote ya miti yaliyopandwa katika kipindi hicho ni hekta 29,194 sawa na asilimia 56.1 ya lengo.
Kwa mujibu wa Mshauri huyo wa Maliasili na Utalii,Mkoa wa Ruvuma unalenga kuanzisha mashamba mapya mawili ya miti ya misaji katika Wilaya za Tunduru na Nyasa.
Kwa upande wake Mratibu wa kuendeleza Program ya mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu(FORVAC) Mkoa wa Ruvuma Marcel Mtunda amesema wameandaa miche ya miti ya biashara aina ya misaji,pine na Eucalyptus ipatayo 4,000,000 ambayo itapandwa maeneo maalum yaliyotengwa na Mkoa yakiwemo Ifinga, Liuli, Liumbe, Upolo,Mpepo,kipiki na Kihangamahuka.
Amesema Mkoa unatekeleza mradi wa kuongeza thamani mazao ya misitu na nyuki kwa kushirikiana na FORVAC na kwamba mradi unatekelezwa katika wilaya zote tano za Mkoa wa Ruvuma.
“Mradi huu utawezesha vijiji kutunza misitu ya hifadhi ya vijiji na kuwawezesha kupata faida kwenye misitu hiyo,hadi sasa wilaya ya Tunduru imeshapata mashine moja ya kuchana mbao ambayo imeanza kufanyakazi katika kijiji cha Sautimoja’’,alisema Mtunda.
Hata hivyo amesema Mkoa kwa kushirikiana na FORVAC imeomba mashine nyingine tatu ili zitumike katika wilaya za Namtumbo,Songea,Mbinga na Nyasa na kwamba mradi utasaidia kupunguza gharama za serikali kutekeleza miradi ya kimkakati ya kujenga shule,zahanati na madawati.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Januari 28,2020
MADABA - RUVUMA
Anwani ya Posta: 38 BARABARA YA KIFAGURO MAGINGO, P.O.BOX 10, 57186 MADABA, SONGEA
Simu: 0252951052
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@madabadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Madaba.Haki zote zimeifadhiwa