Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amesema hayupo tayari kuliingiza Taifa kwenye njaa kwa kuendekeza wafugaji na kwamba ni marufuku wafugaji kuingia kwenye maeneo ya wakulima.
Akizungumza kwa nyakati tofauti na watumishi wa Halmashauri za Madaba na Songea ,Kanali Thomas amesisitiza kuwa Mkoa wa Ruvuma sio Mkoa wa wafugaji bali ni Mkoa wa kilimo ambao unaongoza kitaifa kwa kuzalisha mazao ya chakula .
“Ruvuma sio Mkoa wa wafugaji ni Mkoa wa wakulima,hatuwezi kuliingiza taifa kwenye njaa kwa kuendekeza wafugaji “,alisisitiza RC Thomas.
Amesema operesheni ya kuwaondoa Mifugo yote iliyopo katika maeneo ya wakulima itafanyika katika Mkoa mzima kuanzia Desemba 10 mwaka huu.
Ameuagiza uongozi wa Halmashauri ya Madaba kuwatafuta wafugaji wenye makundi makubwa ya ng,ombe waliopewa dhamana baada ya mifugo yao kukamatwa ikila mazao ya wakulima ili warudi kulipa faini.
Hata hivyo amewapongeza wakulima wa Madaba kutumia busara kubwa kwa sababu wangechukua sheria mkononi yangetokea maafa makubwa kati ya wakulima na wafugaji.
Amesisitiza kuwa wafugaji wote wasiokuwa na kibali waondolewe na kwamba hayupo tayari kuona kundi fulani linakandamiza makundi mengine.
Amesema uchunguzi umebaini kuwa hivi sasa wafugaji hawapandishi Mifugo kwenye magari badala yake wanashushia ng’ombe Wilaya Njombe na kuingia nao kwa miguu mkoani Ruvuma hivyo amemwagiza Kamanda wa Polisi Mkoani Ruvuma kuwadhibiti wafugaji hao .
Ameagiza kuchukuliwa hatua za kisheria kwa mifugo yote inayokamatwa na kwamba watoe taarifa kwake endapo kuna kiongozi yeyote aliyopo chini yake ndani ya Mkoa anakwamisha maagizo yake.
“Hatuwezi kuwa na viongozi wababaishaji ndani ya Mkoa ambao wanadhulumu haki za wananchi ,nilishasema sitaki wafugaji kwenye maeneo ya wakulima “,alisisitiza.
Kwa upande Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Mheshimiwa Menasi Komba amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuwadhibiti wafugaji katika maeneo ya wakulima.
Amesema tayari wamefanikiwa kuondoa mifugo zaidi ya 5000 katika eneo la Kikunja Kata ya Matimira na kwamba kwa kushirikiana na jeshi la polisi wanaendelea kuondoa mifugo hiyo katika maeneo mengine ya wakulima.
Hata hivyo amesema mifugo kwa kiwango kikubwa imedhibitiwa katika Halmashauri hiyo hivyo kupunguza kero kubwa ya uharibifu wa mazao ya wakulima.
Mkoa wa Ruvuma ni kapu la Taifa la chakula nchini ambapo kwa miaka minne mfululizo umeongoza kitaifa katika uzalishaji wa mazao ya chakula.
Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Mkoa wa Ruvuma
Novemba 26,2022
MADABA - RUVUMA
Anwani ya Posta: 38 BARABARA YA KIFAGURO MAGINGO, P.O.BOX 10, 57186 MADABA, SONGEA
Simu: 0252951052
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@madabadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Madaba.Haki zote zimeifadhiwa