Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, Juma Mnwele ameongoza Timu ya Wataalamu wa Halmashauri hiyo na kufanya ziara ya kutembelea Halmashauri ya Wilaya ya Madaba kujionea namna miradi mbalimbali ya maendeleo inavyotekelezwa na Halmashauri hiyo.
Ziara hiyo ya Wataalamu kutoka Mbinga imefanyika leo Aprili 6, 2021 ambapo wamepata nafasi ya kutembelea miradi mikubwa mitatu ya Jengo la Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji (W), Nyumba ya Mkurugenzi na Nyumba 6 za Wakuu wa Idara, miradi ambayo imetekelezwa na inayoendelea kutekelezwa na Halmashauri hiyo ya Wilaya ya Madaba kwa mafanikio makubwa.
Akizungumza wakati wa kikao cha pamoja kati ya Wataalamu wa Halmashauri zote mbili za Mbinga na Madaba, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Bw. Juma Mnwele amesema wanatambua na kuthamini namna Madaba wanavyotekeleza na kusimamia miradi yao hususani jinsi walivyokamilisha ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji na miradi mingine inayoendelea kutekelezwa na wao (Mbinga) wameona ni sehemu nzuri ya kujifunza kupitia wao.
Naye mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba Bw. Shafi Mpenda amemshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga na timu yake ya wataalamu kwa kutembelea Madaba na kuongeza kuwa wamefarikija sana na ujio wa timu hiyo na anaamini baada ya ziara hiyo Mbinga itafanya vizuri zaidi ya walivyofanya wao Madaba katika utekelezaji wa miradi yake ya ujenzi mathalani ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji (W).
Ziara hii ya Timu ya Wataalamu wa Halamshauri ya Wilaya ya Mbinga ni kufuatia Halmashauri hiyo kupokea fedha kiasi cha Tshs. Bilioni Moja kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji, mradi utakaotekelezwa kwa kutumia Force Account, utaratibu unaohusisha Halmashauri kuwa na majukumu na wajibu wa kufanya ununuzi wa vifaa na usimamizi wa ujenzi kupitia kamati mbalimbali badala ya kutumia wakandarasi kama ambavyo Halmashauri ya Wilaya ya Madaba imekamilisha ujenzi wa jengo lake kwa mafanikio makubwa.
Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga inatarajia kuanza ujenzi wa Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji hivi karibuni katika eneo la Kiamili lililopo ndani ya Mji mdogo wa Kigonsera kwa kutumia Force Account, ujenzi ambao utahusisha usimamizi wa karibu wa wataalamu hao kupitia Kamati za Ujenzi, Ununuzi, Ukaguzi na Mapokezi ambapo kupitia ziara hiyo ya kutembelea Halmashauri ya Wilaya ya Madaba, timu hiyo imepata chachu, morali na ari mpya ya kufanya vizuri ili kuleta ufanisi katika usimamizi wa miradi mbalimbali ndani ya Halmashauri hiyo.
Imeandikwa na Salum Said
Afisa Habari Halmashauri ya Mbinga
MADABA - RUVUMA
Anwani ya Posta: 38 BARABARA YA KIFAGURO MAGINGO, P.O.BOX 10, 57186 MADABA, SONGEA
Simu: 0252951052
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@madabadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Madaba.Haki zote zimeifadhiwa