HALMSHAURI ya Wilaya ya Madaba imejipanga kwa Mikakati 17 ya Kitaaluma Mwaka 2024 kwa kuinua ufaulu wa Mtihani wa kumaliza Elimu ya Msingi kutoka asilimia 87.62 hadi asilimia 95.
Afisa Elimu Taaluma wa Halmashauri hiyo Rashid Hashim Pilly ameitaja mikakati hiyo katika Kikao cha Tathimini ya Matokeo ya darasa la saba 2023 ambapo Halmashauri ya Madaba imeshika nafasi ya kwanza Kati ya Halmashauri 8 za Mkoa wa Ruvuma.
Pilly amesema Mikakati hiyo ni pamoja na kuwa na Mitihani miwili ya Utamilifu (Mock) Wilaya kwa darasa la saba na mitihani miwili ya upimaji kwa darasa la nne pamoja na kuwepo kwa kalenda moja kiwilaya ya ufanyikaji wa mitihani ya mihula na nusu muhula.
Amesema kutakuwa na Majaribio ya Wilaya kila mwezi kwa darasa la saba ,utafanyika mtihani ngazi ya Kata na Shule,kufundisha kwa muda waziada kabla ya kuanza masomo saa 1 .00 asubuhi na baada ya masomo saa 9.30 hadi 11.00.
“Kufundisha Madarasa ya Mitihani wakati wa Likizo,siku za sikukuu,siku za Mwisho wa Wiki pamoja na kuwepo kwa makambi mwezi mmoja au zaidi kabla ya mtihani wa Taifa wa darasa la saba”.
Hata hivyo amesema kuzingatia uwepo wa vikao vya tathimini kwa kila ngazi ya shule kila mwezi,kukamilisha mada mwezi Juni kwa darasa la saba na mwezi Agosti kwa darasa la nne.
Amesema zitolewe motisha kwa Walimu na wanafunzi wanaofanya vizuri katika taaluma,pamoja na kuwepo kwa vikao vya wazazi na wadau mbalimbali wa elimu na kujadili maendeleo ya elimu.
“Kuwepo kwa chakula cha wanafunzi na walimu,kuwepo kwa mabaraza ya wanafunzi kwa kila shule,kuboresha mazingira ya shule yatakayovutia wanafunzi,michezo,bendi ya shule”.
“Kila shule ihakikishe inadhibiti utoro wa wanafunzi pamoja na kuwepo kwa sanduku la maoni kwa kila shule na liwekwe mahali ambapo ni huru kwa wanafunzi kuweka maoni yao”.
Kutoka kitengo cha Mawasiliano Halmashauri ya Madaba
Disemba 5,2023.
MADABA - RUVUMA
Anwani ya Posta: 38 BARABARA YA KIFAGURO MAGINGO, P.O.BOX 10, 57186 MADABA, SONGEA
Simu: 0252951052
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@madabadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Madaba.Haki zote zimeifadhiwa