MKUU wa Wilaya ya Songea Mheshimiwa Pololeti Mgema ametoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Madaba kusimamia fedha za miradi kwa uaminifu na uadilifu, ikiwemo Madarasa ambayo ameelekeza kuwa yakamilike kwa wakati.
Hayo ameyasema katika Kikao cha Baraza la Madiwani kilichopokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya halmashauri yaliyotekelezwa katika robo ya nne ya mwaka wa fedha 2020/2021. Kikao hicho kilichofanyika tarehe 21/08/2021 katika Ukumbi wa Halmashauri.
Mhe. Pololeti Mgemaalisema kuwa, fedha zinazoletwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya wananchi zisimamiwe kwa uaminifu na kwa uadilifu ili Halmashauri ya Madaba iendelee kutekeleza miradi yenye viwango vinayolingana na fedha zinazoletwa kutoka Serikalini.
Mh. Pololeti Mgema amesema, fedha zilizotolewa kwa ajili ya Madarasa shilingi milioni kumi na mbili na laki tano (12,500,000/=) zinaweza kukamilisha majengo ambayo yameanzishwa kwa nguvu za wananchi. Aidha amesema kuwa, madarasa yaliyoletewa shilingi milioni 20 (kwa kila darasa) zitumike kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mapya kuanzia msingi hadi kumaliza bila kuwachangisha wananchi.
Alimuagiza Mkurugenzi akisema,“Fuatilia mahali ambapo tumejenga madarasa ambapo wananchi waliambiwa watoe tofali na nguvu zingine. Kile ambacho walichangia kibadilishwe kuwa gharama na iwe sehemu ya kuokoa fedha kwenye mradi huo, tuokoe fedha kwa sababu wananchi walichangia”alisisitiza.
Hata hivyo amelaani kitendo cha kusimamisha kazi ya ujenzi wa madarasa ya shule ya msingi katika kijiji cha likalangilo kwa sababu wananchi hawajaleta tofali za kutosha na amemwagiza Mkurugenzi kufuatilia swala hilo.
“Wananchi wanajitoa katika shughuli za maendeleo na Waheshimiwa Madiwani wanajitoa, huo ni msaada wako maana umekuja kwenye Halmashauri ambayo Madiwani ni wamoja hakuna migogoro ya wenyewe kwa wenyewe wala migogoro ya Madiwani na watumishi, uwaweke watumishi wafanye kazi kwa bidii ili serikali isipate hasara ya kulipa mtumishi mvivu”.amesisitiza Mgema.
Amesema Serikali kwasasa inaleta fedha ya miradi kwa kiwango kikubwa ikiwemo milioni 500 zilizoletwa kwa kila Halmashauri lakini Madaba imetengewa bilioni moja kwa ajiji ya matengenezo ya barabara. Fedha hizi zisimamiwe vizuri.
Mh. Mgema ametoa maelelekezo katika Baraza hilo kuwahamasisha wananchi kujiunga na CHF iliyoboreshwa ili kupata huduma bora ya afya kwa shilingi elfu thelatini kwa mwaka, na kumwagiza Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo kuhakikisha kuwa, kituo cha Afya Mtyangimbole kuanza kufanya kazi na huduma zote zitolewe kwa sababu kituo hicho kimekwisha kukamilika.
Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Bw. Sajidu Idrissa Mohamed katika Baraza hilo ikiwa ni kikao chake cha kwanza amemshukuru Rais kwa kumuona na kumleta Madaba, ameomba ushirikiano kwa Wataalamu ili kuhakikisha Halmashauri inasonga mbele katika Nyanja zote.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mhe. Teophanesi Mlelwa wakati akifunga kikao hicho ameahidi kutoa ushirikiano kwa Mkurugenzi mpya katika utendaji wa kazi na amewaomba watumishi na Waheshimiwa Madiwani kumpa ushirikiano ili kuhakikisha Halmashauri hiyo inaendelea kufanya vizuri.
Imeandaliwa na Aneth Ndonde
Afisa Habari Halmashauri ya Mdaba
Agosti 22,2021
MADABA - RUVUMA
Anwani ya Posta: 38 BARABARA YA KIFAGURO MAGINGO, P.O.BOX 10, 57186 MADABA, SONGEA
Simu: 0252951052
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@madabadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Madaba.Haki zote zimeifadhiwa