Maadhimisho ya kilele cha Siku ya Kimataifa ya Wazee Duniani mwaka 2025 yamefanyika leo, Oktoba 1, 2025, katika Ukumbi wa Songea Club, Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, yakiambatana na kaulimbiu isemayo “Wazee Tushiriki Uchaguzi kwa Ustawi wa Jamii Yetu.”
Sherehe hizo zimekusanya mamia ya wazee kutoka mikoa mbalimbali nchini, zikiwa na lengo la kuhamasisha ushiriki wao katika mchakato wa kidemokrasia pamoja na kuenzi mchango wao katika historia na maendeleo ya taifa.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Bi. Marry Makondo, alisema wazee ni hazina ya hekima na dira ya taifa, hivyo jamii ina wajibu wa kuwatunza na kuwathamini.
Kwa upande wake, Mratibu wa Huduma kwa Wazee kutoka TAMISEMI, Bw. Haroun Yunus Haroun, alieleza kuwa serikali imefanikiwa kuwatambua wazee kwa kuwapatia vitambulisho pamoja na bima ya afya. Aidha, halmashauri 184 nchini zimeanzisha jumla ya madirisha 4,094 ya huduma kwa wazee, hatua inayoongeza upatikanaji wa huduma rafiki.
Naye, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee la Taifa, Bw. David Sendo, alisisitiza kuwa mshikamano na amani ya taifa ni matunda ya hekima ya wazee waliotangulia, hivyo vijana wanapaswa kujifunza na kuthamini mafunzo yao.
Akizungumza kwa niaba ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Naibu Katibu Mkuu, Wakili Amon Mpanju, alihimiza jamii kupinga vitendo vya ukatili dhidi ya wazee huku akisisitiza usawa na heshima kwa makundi yote ya kijamii.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas, aliwahimiza wananchi kutumia kaulimbiu ya mwaka huu kama mwongozo wa kuichagua serikali ambayo inajali, sikivu na kutambua changamoto za wazee. Alisisitiza kuwa wazee wanastahili heshima, ushirikishwaji katika masuala ya kijamii na kitaifa, ikiwemo upatikanaji wa huduma muhimu.
MADABA - RUVUMA
Anwani ya Posta: 38 BARABARA YA KIFAGURO MAGINGO, P.O.BOX 10, 57186 MADABA, SONGEA
Simu: 0252951052
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@madabadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Madaba.Haki zote zimeifadhiwa