Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Dr. Abubakary Zuberi bin Zuberi, amewasili mkoani Ruvuma kwa ziara ya kidini yenye lengo la kuimarisha ustawi wa jamii ya Kiislamu na kuhimiza mshikamano miongoni mwa waumini. Ziara hii ni sehemu ya juhudi za Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) katika kusogeza huduma na uongozi wa kiroho karibu na ngazi za chini.
Mapokezi ya Mufti Mkuu katika Halmashauri ya Wilaya ya Madaba, yakihudhuriwa na viongozi wa dini, serikali, na mamia ya waumini waliokusanyika kumpokea kwa shangwe na heshima. Sheikh wa Mkoa wa Ruvuma, Ramadhani Mwakilima, aliongoza mapokezi hayo na kueleza kuwa ujio wa Mufti Mkuu unaongeza ari kwa viongozi wa dini na waumini katika kushiriki shughuli za maendeleo na uimarishaji wa imani.
Akitoa salamu zake, Sheikh Mwakilima alieleza kuwa ziara hiyo imekuja wakati muafaka, kwani inawapa waumini nafasi ya kupata maelekezo ya moja kwa moja kutoka kwa uongozi wa kitaifa wa BAKWATA, sambamba na kushirikiana katika kufanikisha miradi ya kijamii inayotekelezwa na taasisi hiyo. Aliongeza kuwa ni fursa ya kuimarisha mshikamano wa kidini na kijamii.
Mufti Mkuu, aliwashukuru wananchi wa Ruvuma kwa mapokezi ya upendo na mshikamano, akisisitiza kuwa umoja wa Waislamu ni chachu ya maendeleo ya kitaifa. Alihimiza viongozi wa dini kuendelea kuwa daraja la maelewano, huku akisisitiza jukumu la waumini kushiriki katika kulinda maadili, amani na ustawi wa jamii.
Akiwa mkoani Ruvuma, Mufti Mkuu atazuru wilaya za Songea, Namtumbo, Tunduru na Nyasa, ambako atakutana na viongozi wa dini, waumini na watendaji wa serikali. Aidha, atakagua na kuzindua miradi mbalimbali ya Kiislamu kama misikiti, shule, na vituo vya malezi ya watoto wa Kiislamu (madrasah), ikiwa ni ishara ya kuunga mkono maendeleo ya elimu na huduma za kijamii.
Ziara hii ni sehemu ya mpango mpana wa BAKWATA wa kujenga uhusiano thabiti kati ya makao makuu na viongozi wa mikoa, pamoja na kuhakikisha taasisi za Kiislamu zinatoa mchango chanya katika maendeleo ya taifa. Mufti Mkuu anatarajiwa kuhitimisha ziara yake kwa kutoa hotuba kwa viongozi wa dini na waumini kuhusu nafasi ya Waislamu katika kulinda amani na kulea kizazi chenye maadili bora