Halmashauri ya Wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma imepokea jumla ya meza na viti 40 kwa ajili ya Shule ya Sekondari Mtyangimbole kutoka Benki ya CRDB Kanda ya Kusini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za benki hiyo kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuboresha sekta ya elimu nchini.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba, Wakili Sajidu Idrisa Mohamed, ameishukuru Benki ya CRDB kwa mchango huo muhimu na kuipongeza kwa kujali juhudi za Serikali katika kuhakikisha elimu bora inapatikana kwa wanafunzi wote nchini.
Aidha Mkurugenzi, amewataka wanafunzi wa shule hiyo kutunza viti na meza walizokabidhiwa, huku akimwagiza Afisa Elimu Sekondari kuhakikisha hatua kali zinachukuliwa dhidi ya wanafunzi watakaoharibu mali za shule.
Pia, amesisitiza kuwa ujenzi wa Shule ya Sekondari Mtyangimbole yenye thamani ya shilingi milioni 560 ni uthibitisho wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha miundombinu ya elimu na kuwaondolea wanafunzi adha ya kutembea umbali mrefu kufuata masomo.
Kwa upande wake, Meneja wa CRDB Kanda ya Kusini, Denis Mwoleka, amesema benki hiyo imeanzisha kampeni ya miaka mitatu ijulikanayo kama “Keti Jifunze”, yenye lengo la kusaidia shule mbalimbali nchini kwa kutoa meza na viti, ili kuunga mkono jitihada za Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuendeleza sekta ya elimu.
Mwoleka ameongeza kuwa kampeni hiyo itazifikia shule zote katika kila Halmashauri nchini, ili kuhakikisha kila mwanafunzi anapata mazingira bora ya kujifunzia na kuimarisha ubora wa elimu.
MADABA - RUVUMA
Anwani ya Posta: 38 BARABARA YA KIFAGURO MAGINGO, P.O.BOX 10, 57186 MADABA, SONGEA
Simu: 0252951052
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@madabadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Madaba.Haki zote zimeifadhiwa