Wakuu wa Idara wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma wamepatiwa mafunzo maalumu kutoka Benki ya CRDB kuhusu huduma mbalimbali za kifedha na fursa za mikopo inayotolewa na benki hiyo, katika jitihada za kuongeza uelewa wa watumishi kuhusu masuala ya fedha na maendeleo.
Mafunzo hayo yalifanyika katika Ofisi za Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, yakiongozwa na Meneja wa Kanda ya Kusini wa Benki ya CRDB, Ndg. Denis Mwoleka, ambaye aliambatana na timu ya maofisa wa benki hiyo.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Ndg. Mwoleka alisema lengo kuu ni kuwajengea uwezo watumishi wa umma kuhusu namna bora ya kutumia huduma za benki kwa maendeleo yao binafsi na taasisi wanazozitumikia.
Katika mafunzo hayo, washiriki walipatiwa elimu kuhusu mikopo ya watumishi, mikopo ya wajasiriamali, mikopo ya kilimo, pamoja na mikopo ya vyombo vya usafiri. Aidha, walifundishwa umuhimu wa kuweka akiba kama msingi wa ustawi wa kifedha.
Washiriki walieleza kufurahishwa na mafunzo hayo wakisema yamewapanua uelewa kuhusu fursa zilizopo ndani ya Benki ya CRDB, ambazo zinaweza kuchochea mafanikio ya miradi ya maendeleo ya Halmashauri na wananchi kwa ujumla.
Katika kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja, Benki ya CRDB pia ilikabidhi keki maalumu kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba, ikiwa ni zawadi kwa watumishi wote kama ishara ya upendo, amani, na ushirikiano thabiti kati ya benki hiyo na halmashauri.
MADABA - RUVUMA
Anwani ya Posta: 38 BARABARA YA KIFAGURO MAGINGO, P.O.BOX 10, 57186 MADABA, SONGEA
Simu: 0252951052
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@madabadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Madaba.Haki zote zimeifadhiwa